POLISI WASHIKILIWA KIFO CHA BODABODA DODOMA
- Habari
- July 21, 2025
- No Comment
- 49
Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma linawashikilia askari wake wawili kwa tuhuma za kumjeruhi kwa risasi na kusababisha kifo cha kijana mmoja aitwaye Frank Sanga (32), mkulima na mkazi wa Mtaa wa Kusenha, Kata ya Matumbulu, Jijini Dodoma.
Akizungumza na waandishi wa habari leo ofisini kwake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Gallus Hyera amesema tukio hilo limetokea siku ya Jumamosi, Julai 19, 2025, majira ya saa 7:30 mchana, wakati askari hao wakiwa katika doria ya kawaida ya kuzuia uhalifu katika maeneo ya Jiji la Dodoma.
Kwa mujibu wa Kamanda Hyera, askari hao walimkamata mtu mmoja aitwaye Mathias Julias Choma (32), mkazi wa Mpwayungu, Wilaya ya Chamwino, kwa makosa ya usalama barabarani ikiwemo kutovaa kofia ngumu, kutokuwa na leseni ya udereva, pamoja na kuendesha pikipiki isiyokuwa na hali nzuri ya kiusalama (mbovu) ambapo Mathias aliwaomba Askari kutumia simu kuwasiliana na ndugu zake, baada ya kupata taarifa, baadhi ya ndugu na jamaa walifika katika eneo hilo na silaha za jadi huku wakiwa kwenye hali ya hasira na ndipo wakaanza kufanya vurugu kwa lengo la kumkomboa kwa nguvu ndugu Yao ili asipelekwe kituo Cha polisi.
Kamanda huyo ameeleza kuwa, katika vurugu hizo, askari mmoja alifyatua risasi kwa lengo la kujihami, ambapo risasi hizo zilimjeruhi Frank Sanga katika paja la mguu wa kushoto na sehemu ya nyonga (ugoko), mjeruhi alikimbizwa Hospitali ya DCMC kwa matibabu, lakini alifariki dunia akiwa anaendelea kupatiwa matibabu.
