
HATMA KESI YA LISSU KUJULIKANA SEPTEMBA 15
- Habari
- September 11, 2025
- No Comment
- 25
Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, ambaye anakabiliwa na kesi ya uhaini, leo Septemba 11, 2025 amewasilisha hoja zake za mwisho katika Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam. Uamuzi wa shauri hilo umepangwa kutolewa Jumatatu, Septemba 15, 2025 saa 3 asubuhi na jopo la Majaji watatu wakiongozwa na Jaji Dustan Nduguru, pamoja na Jaji James Karayemaha na Jaji Ferdinand Kiwonde. Hukumu hiyo itabainisha iwapo Lissu ataendelea kubaki mahabusu au ataachiwa huru.
Katika hoja zake, Lissu ameomba kesi hiyo ifutwe akidai kuwa mwenendo wake tangu ulipoanza Kisutu ulikuwa na mapungufu makubwa ya kisheria na kiutaratibu. Amesema upungufu huo umeondoa uhalali wa shauri kuendelea, kwani umeathiri misingi ya usawa na haki za msingi za mtuhumiwa. Kwa siku nne mfululizo, Lissu amewasilisha hoja akifafanua jinsi kasoro hizo zilivyoathiri haki yake ya kupata usikilizwaji wa haki na kwa njia sahihi.
Kwa upande mwingine, Jamhuri imepinga hoja hizo kwa msimamo kuwa makosa yaliyotajwa ni ya kawaida ya kibinadamu na hayatoshi kufutwa kwa kesi nzima. Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, kasoro hizo zinaweza kurekebishwa na shauri likaendelea kama kawaida. Hali hii sasa imeweka wasiwasi na matarajio makubwa miongoni mwa wananchi na wadau wa siasa, huku macho yote yakielekezwa kwa jopo la Majaji ambalo litatoa uamuzi muhimu unaoweza kuathiri siasa na mustakabali wa Tundu Lissu.