
SGR INAVYOOKOA GHARAMA NA MUDA KWA WASAFIRI
- Habari
- March 23, 2025
- No Comment
- 63
Reli ya Mwendokasi SGR imewezesha wananchi kupata huduma ya usafiri na usafirishaji wenye Staha na gharama nafuu ambazo kila mwananchi anazimudu.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dodoma, kuhusu mafanikio yanayotokana na uwekezaji wa Serikali katika reli kwa kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) Masanja Kadogosa amesema moja ya faida za SGR ni kupunguza muda wa safari kutoka Dar – Dodoma ni masaa 3 – 4 ikilinganishwa na masaa 9 – 12 kwa mabasi.
“Uendeshaji wa Reli ya SGR bila ruzuku ya Serikali, kuchochea ukuaji wa sekta nyingine za kiuchumi, upatikanaji wa ajira kwa Watanzania ambapo ajira zaidi ya 30,176 za moja kwa moja na ajira zaidi ya 150,880 zisizo za moja kwa moja zimezalishwa kupitia miradi hii, utunzaji wa mazingira ambapo takribani tani 14,327.3 za hewa ya ukaa (CO2) zimepungua, kusafirisha mzigo mkubwa kwa mara moja,” alisisitiza Masanja
Aidha, Kadogosa amesema kuanza huduma za usafirishaji wa kwa treni za mizigo kutaongeza uwezo wa usafirishaji ambapo treni moja itabeba kiasi cha tani 3,000 kwa wakati mmoja, hii itapelekea kupungua kwa gharama za usafiri na hivyo kupungua kwa bei za bidhaa sokoni na kupunguza matumizi ya fedha za kigeni.
Akitolea mfano mafankio mengine amesema ni kusafirisha abiria milioni 2.1 tangu kuanza kwa shughuli za usafirishaji.
Sanjari na hayo, SGR imewezesha kupungua kwa gharama za matengenezo ya barabara kutokana na mzigo mkubwa kusafirishwa kwa njia ya reli, kuchangia ufanisi wa bandari na ukuaji wa sekta zingine ikiwemo nishati, kilimo na viwanda, na kuchagiza ukuaji wa miji katika maeneo yaliyopo katika ushoroba wa reli.