
WAZIRI WA ULINZI NA JKT ASHIRIKI MKUTANO WA VIONGOZI WANAWAKE
- Habari
- January 11, 2025
- No Comment
- 97
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mheshimiwa Dkt. Stergomena Lawrence Tax (Mb) tarehe 11 Januari 2025, Hoteli ya Serena jijini Dar-es-salaam, ameshiriki na kuwa Mgeni Rasmi wa Kongamano la Pili la Viongozi Wanawake lijulikanalo kama Women’s Leadership Summit na kuwaasa washiriki wa Kongamano hilo kuziishi ndoto zao na kuwa na uthubutu katika kutimiza malengo yao ili kuleta mafanikio kwenye nyanja mbalimbali katika jamii.
Kongamano hilo la viongozi wanawake limeandaliwa na vijana wa kike Maura Mgaya na mwenzake Nioma Semega limeshirikisha vijana wa kike wenye shauku ya kufikia mafanikio katika ndoto zao kutoka baadhi ya Shule za Sekondari, Vyuo na Sekta binafsi.
Akizungumza katika Kongamano hilo, Waziri Tax, amewataka vijana kujituma na kushirikiana katika kuweka bidii kwa kila nafasi wanayoaminiwa na wahakikishe wanafanya uchaguzi sahihi wa marafiki hasa wenye ndoto kubwa na fikra Chanya ili kwao wapate changamoto sahihi kuelekea mafanikio ya ndoto zao “Ukitaka Kwenda haraka nenda peke yako, ukitaka Kwenda mbali nenda na wenzako” alisisitiza Dkt Tax.
Aidha, Waziri wa Ulinzi na JKT, Dkt Stergomena Tax amewaambia vijana hao wa kike kuwa Vijana ni viongozi wa kesho katika Jamii ya Tanzania, akawataka kujua wana sehemu gani katika jamii na mchango gani jamii inawategemea kuleta tija, pia akawakumbusha kuwa uongozi ni kuacha alama katika jamii iliyokuzunguka. Waziri Tax pia akawasisitiza washiriki wa Kongamano hilo kuwa uongozi ni pamoja na kuwawezesha wale wote walio pamoja nawe katika maisha ya kila siku.
Dkt. Stergomena Tax akawapongeza waandaaji wa Kongamano hilo na timu yao, kwa uthubutu wa kuandaa tamasha hilo la viongozi wa kike kwa mafanikio.