
KITUO CHA RELI DODOMA KUBORESHA HUDUMA ZAKE
- Habari
- June 19, 2025
- No Comment
- 42
Wataalamu wanaosimamia Kituo cha Reli ya Mwendokasi (SGR) cha Jijini Dodoma, Samia Suluhu Hassan, wanaendelea na maboresho ya huduma kwenye kituo hicho ili kukidhi matumizi sahihi ya mabehewa yanayobeba abiria takribani 7,000 kwa siku, wanaosafiri kutoka Dar es Salaam kuja Dodoma na kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam.
Hayo yamebainishwa na Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma Bw. Kaspar K. Mmuya leo Juni 19, 2025 alipotembelea Banda la Shirika la Reli Tanzania (TRC) linalopatikana katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi yanayoendelea katika Viwanja vya Bustani ya Mapumziko Chinangali Jijini Dodoma.
“Wataalam wangu wameniambia wanaendelea kuboresha huduma ili kukidhi matumizi sahihi ya Mabehewa haya ya ‘Royal’, ‘Bussines’ na ‘Economy’. Sisi wenye dhamana ya kusimamia maendeleo ya Mkoa wa Dodoma tunapata ‘Feedback’ kuhusu huduma wanazozipata kama zinafana na hadhi ya mabehewa hayo. Tunategemea tutoe huduma bora kwa kila anayetumia miundombinu yetu ambayo Serikali imewekeza.”
Ameongeza kuwa, ujio wa watu wengi ndani ya Mkoa huu ni fursa kibiashara hususan katika kuinua uchumi hivyo, ametoa hamasa kwa wakazi wa Jiji hili kuchangamkia fursa hizo kwani kila anayeingia Mkoani hapa, kuna huduma anakayohitaji ambayo itainua uchumi wa mtu mmoja mmoja na Mkoa kwa ujumla.
Katibu Tawala Mkoa ametembele Mabanda yaliyo chini ya Wizara ya uchukuzi ikiwa ni pamoja na Banda la Wizara yenyewe, Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA), Chuo cha Usafirishaji cha Taifa, Shirika la Reli Tanzania (TRC), Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) pamoja na Shirika la Utangazaji Nchini (TBC).
Maonesho hayo kulekea Kilele cha Siku ya Utumishi wa Umma Duniani ifikapo Juni 23, 2025, huanza Juni 16 kila mwaka yakilenga kusogeza huduma karibu na wananchi kutokana na kukusanyika kwa Taasisi zote za Umma kwenye eneo moja huku zikitoa huduma kwa wananchi.
Kaulimbiu: “Himiza Matumizi ya Mifumo ya Kidijiti ili Kuongeza Upatikanaji wa Taarifa na Kuchangia Uwajibikaji”.