
WAZIRI NDEJEMBI AAGIZA UKUTA KUBOMOLEWA KIGOGO
- Habari
- February 15, 2025
- No Comment
- 77
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Deogratius Ndejembi, ametoa siku mbili kuanzia leo Februari 15, 2025, kwa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kuvunja sehemu ya ukuta wa kiwanja namba P18618 kilichopo Kigogo, Dar es Salaam, baada ya mmiliki wake kushindwa kuwasilisha nyaraka za umiliki halali.
Waziri Ndejembi amesisitiza kuwa uchunguzi wa wataalamu kupitia Kamishna wa Ardhi ulibaini kuwa Kampuni ya Nizar Food ilijiongezea ukubwa wa eneo lake kinyume cha sheria na kulijengea ukuta na hivyo sehemu ya ukuta huo unapaswa kubomolewa ili kulinda maeneo ya wazi.
Ikumbukwe kuwa, januari 21 mwaka huu Waziri Ndejembi alifika katika eneo hilo lenye mgogoro wa muda mrefu kati ya wananchi na mmiliki wa kiwanja hicho kampuni ya Nizar Food ambapo aliwataka wamiliki hao kuwasilisha nyaraka zinazoonesha uhalali wa kuongeza ukubwa wa kiwanja hicho, lakini hawakufanya hivyo ndani ya muda aliotoa.
✍️| Kastul Elias